6 Desemba 2025 - 11:10
Je, Senario ya Maafa ya Al-Fasher Inarejelewa Tena Katika Mji wa Babanusa, Sudan?

Shirika la Umoja wa Mataifa limeonya kuwa hali ya kibinadamu katika mji wa Babanusa, uliopo katika jimbo la West Kordofan nchini Sudan, iko katika hatari kubwa ya kushuhudia janga kama lililotokea katika mji wa Al-Fasher, Kaskazini mwa Darfur, endapo hali ya sasa itaendelea kuzorota.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- mji wa Babanusa umekuwa chini ya mzingiro wa vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) kwa wiki kadhaa sasa. Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa kuzidi kwa hali ngumu ya kibinadamu katika mji huo kunaweza kusababisha maafa makubwa ya kibinadamu kama yale ya Al-Fasher.

Jeshi la Sudan limethibitisha kuwa vikosi vya RSF vimekuwa vikiushambulia mji wa Babanusa kwa kutumia mizinga ya kivita na ndege zisizo na rubani (drones) za kimkakati, hata hivyo limekanusha taarifa zinazodai kuwa mji huo umeanguka rasmi mikononi mwa wapiganaji hao.

Mji wa Babanusa una umuhimu mkubwa wa kijeshi na kimkakati, kwani unachukuliwa kuwa kitovu muhimu cha udhibiti wa njia za kusafirishia majeshi na vifaa vya kijeshi. Idadi ya wakazi wa mji huo inakadiriwa kuwa takribani watu 300,000.

Jeshi la Sudan limesema kuwa bila kudhibiti Babanusa, haiwezekani kufikia sehemu kubwa za Darfur au maeneo mengine ya Kordofan, jambo ambalo linaifanya mji huo kuwa nguzo muhimu ya kimuundo katika mikakati ya kijeshi ya serikali. Hivyo basi, kuanguka kwa Babanusa mikononi mwa RSF kutakatisha njia kuu zote za usambazaji wa jeshi.

Kwa upande mwingine, kwa vikosi vya Rapid Support Forces, kuudhibiti mji wa Babanusa kuna fungua njia ya moja kwa moja kuelekea mji wa Al-Ubayyid (El-Obeid) katika Kaskazini mwa Kordofan, hatua ambayo inaweza kubadilisha kabisa mizani ya vita katika eneo hilo.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha